Mtu mmoja amefariki na wengine wanane wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu katika eneo la Kingolwira Manispaa ya Morogoro barabara kuu ya Morogoro – Dar es salaam.
RPC wa Morogoro, Alex Mkama amesema ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo ambapo gari moja lililobeba mafuta ya petroli (Howo) lililokuwa linatokea Dar es salaam kuelekea Morogoro liligongana na basi la abiria la Kampuni ya Johanvia linalofanya safari zake Musoma – Dar es salaam na kisha basi hilo kuligonga gari la Polisi lililokuwa limepaki pembezoni mwa barabara.
RPC Mkama amesema aliyefariki katika ajali hiyo ni Mtuhumiwa Yohana Mwamlima (40) ambaye inadaiwa alikuwa akitokea Musoma kupelekwa Dar es salaam, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva wa gari la mafuta, Nkandi Konokwa (61) ambaye alikuwa anaendesha gari kwa mwendokasi na kwa sasa anashikiliwa na Polisi.