Ujumbe kutoka Jumuiya ya ECOWAS ukiongozwa na aliyewahi kuwa kiongozi wa kijeshi nchini Nigeria, Abdulsalami Abubakar, na Sultan wa Sokoto Muhammad Sa’ad Abubakar III walizuru jijini Niamey kukutana na viongozi wa jeshi lakini pia rais Mohammed Bazoum.
Ujumbe huu umekuja kujaribu kuzungumza na jeshi wakubali kurejesha madaraka kwa raia, wakati huu ripoti zikisema hawakufanikiwa kukutana na jeshi na rais Bazoum.
Msemaji wa rais wa Nigeria Bola Tinubu, Abdulaziz Abdulaziz, ameiambia RFI Hausa kuwa, ujumbe mwingine unazuru Libya na Algeria, nchi ambazo pia zinapakana na Niger, kutafuta uungwaji mkono.
Algeria na Libya, ambazo hazipo kwenye Jumuiya ya ECOWAS hazijafunga mipaka yao na Niger.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaeleza kuwa iwapo Ecowas itahitaji kutumia nguvu za kijeshi nchini Niger, itategemea pakubwa kwa nchi ya Nigeria ambayo ina wanajeshi 223,000 pamoja na ndege za kivita za kisasa na helikopta za kujihami.
Senegal siku ya Alhamis ilisema kwamba itashiriki iwapo ECOWAS itachagua kutumia jeshi nchini Niger.
Waziri wa mambo ya kigeni wa nchini humo Aissata Tall Sall aliwaambia waandishi wa habari jijini Dakar kuwa Senegal itaenda kulingana na matakwa ya Ecowas.
Nchi zengine za Jumuiya hiyo tayari zimetangaza hazitashiriki iwapo suala ya kutumia nguvu za kijeshi nchini Niger litaafikiwa.