Zaidi ya watu 60 wanahofiwa kufariki baada ya mashua iliyokuwa imebeba wahamiaji kupatikana karibu na Cape Verde huko Afrika Magharibi.
Watu 38 wakiwemo watoto waliokolewa huku picha zikiwaonyesha wakisaidiwa kufika ufukweni, wengine kwenye machela katika kisiwa cha Sal.
Takriban wote waliokuwa kwenye mashua hiyo, ambayo ilikuwa baharini kwa zaidi ya mwezi mmoja, inadhaniwa walikuwa wanatoka Senegal.
Maafisa wa Cape Verde wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kimataifa kuhusu uhamiaji ili kusaidia kuzuia hasara zaidi ya maisha.
Boti hiyo ilionekana kwa mara ya kwanza Jumatatu, polisi waliambia shirika la habari la AFP. Taarifa za awali zilidokeza kuwa boti hiyo ilikuwa imezama lakini baadaye ikafafanuliwa kuwa ilipatikana ikiyumba.
Boti ya mbao ya mtindo wa pirogue ilionekana karibu kilomita 320 (maili 200) kutoka Sal, sehemu ya Cape Verde, na mashua ya uvuvi ya Uhispania, ambayo ilitahadharisha mamlaka, polisi walisema.
Walionusurika ni pamoja na watoto wanne wenye umri wa kati ya miaka 12 na 16, msemaji wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) alisema.
Boti hiyo iliondoka katika kijiji cha wavuvi cha Senegal cha Fasse Boye mnamo Julai 10 ikiwa na watu 101, wizara ya mambo ya nje ya Senegal ilisema Jumanne, ikinukuu manusura.
Moda Samb, afisa aliyechaguliwa katika kijiji hicho, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba karibu wote waliokuwemo kwenye boti hiyo wamekulia katika jamii na kwamba baadhi ya familia za eneo hilo bado zinasubiri kusikia kama jamaa zao walikuwa miongoni mwa walionusurika.