Waziri wa Kilimo Hussein Bashe @bashehussein amesema sio kweli kwamba zao la vanilla linauzwa kwa kilo Tsh.mil 1.5 ambapo amesema taarifa hizo ni za uongo huku akiwataka Waandishi wa Habari kuisaidia Serikali kufikisha taarifa sahihi kwa Wakulima kuhusu bei za mazao na taarifa nyingine za kilimo.
Bashe amesema hayo leo Ikulu Dar es salaam wakati akiongea na Viongozi pamoja na Wahariri kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari kuhusiana na Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF-Afrika Food Systems Summit 2023), unaotarajiwa kufanyika Sept 05-08,2023 Jijini Dar es salaam.
Bashe amesema “Nitaanza na swali la Mwandishi aliyeuliza je vanilla inauzwa Mil 1.5 ni uongo, nimesikia iliandikwa gazeti la Mwananchi ni vizuri kutochukua taarifa ambazo hazina uthibitisho, kwakuwa nyinyi ni Waandishi ni vizuri Vyombo vya Habari mkalipia ada kidogo kujiunga kwenye International Commodity Platform Prices ambazo zinawasaidia kuona bei za bidhaa Duniani kote lakini zipo platform kama Business Insiders ukiingia unaweza kuona bei halisi ya bidhaa fulani Duniani kwa wakati fulani”
“Tanzania tunazalisha vanilla kwa kiwango kidogo, Mikoa kama ya Kagera na Mikoa ya Kilimanjaro na vanilla ni zao ambalo lina eneo sana soko lake ni kama pareto, pareto sisi Tanzania ni Wazalishaji wa pili Duniani lakini tunazalisha tani Elfu 2 hadi Elfu 3 anayeongoza Duniani anazalisha tani Elfu 8”
“Kwahiyo vanilla zipo Nchi zimeshapiga hatua sana Duniani zinazofanya vizuri kwenye zao hili, vanilla ilipanda bei hapa miaka miwili mitatu baada ya Nchi kama Madagascar zilipokumbwa na vimbunga kwasababu wao ni Wazalishaji wakubwa na sisi ikasaidia Wakulima wetu kupata bei nzuri, kwahiyo bei ya Tsh. mil 1.5 haipo Duniani, bei ya laki 5 haipo Duniani”