Rais wa Kenya William Ruto na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga wameungana katika ukosoaji wao wa uamuzi wa mahakama ya juu zaidi wa wiki jana ambao unaoruhusu jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja kusajili Vikundi vya harakati zao nchini Kenya.
Rais Ruto sasa ameapa kuwa kamwe hataruhusu ndoa za watu wa jinsia moja nchini Kenya, ambapo alisema ‘inakwenda kinyume na tamaduni na imani za kidini za nchi hiyo’.
Haya yanajiri baada ya siku ya Jumanne, mahakama ya juu kutupilia mbali ombi la Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma lililotaka kupinga uamuzi wa mahakama kuhusu usajili wa LGBTQ+.
Katiba ya Kenya inaruhusu ndoa kati ya watu wa jinsia tofauti pekee, huku kanuni ya adhabu inaadhibu ngono ‘kinyume na utaratibu wa asili’ kwa kifungo cha hadi miaka 14 jela.
Rais Ruto amewataka wakenya kutokuwa na wasiwasi akiwahakikishia kwamba uamuzi huo hautatekelezwa nchini humo huku akiwataka viongozi wa dini kusimama kidete na kupigania maadili ya taifa hili.