Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Mashaka Biteko amelipongeza Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa usimamizi makini na hatua kubwa iliyofikiwa kwenye ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, ambao mpaka sasa umefikia asilimia 91.72.
Mhe.Dkt Biteko ameyasema hayo leo Septemba 16, 2023 alipofanya ziara katika mradi huo wa kimkakati na kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya kazi kubwa ya kuusimamia kwa karibu mradi huu.
“Tunashukuru sana Serikali pamoja na wizara na TANESCO kwa kuhakikisha ujenzi unaenda kwa kasi licha ya kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa umeme unaosababishwa na kupungua kwa kina cha maji kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme”. Alisema Mhe. Biteko.
Aliongeza kuwa kwa sasa umuhimu ni watanzania wapate umeme wa uhakika ambapo suluhisho mojawapo ni kukamilika kwa mradi wa JNHPP.
Mradi wa bwawa la kufua umeme wa Julius Nyerere ulianza ujenzi wake Disemba 12, 2018 na unagharimu kiasi cha shilingi Trilioni 6.5 na hadi sasa mkandarasi amekwishalipwa kiasi cha shilingi trilioni 5.6 cha malipo yote.
Ziara hii inakuwa ya kwanza kutembelea mradi huu wa kimkakati wa Julius Nyerere tangu ateuliwe na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.