Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu wananchi katika Wilaya ya Nachingwea, Mkoani Lindi juu ya changamoto ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji jambo linaloathiri hali ya usalama pamoja na uzalishaji Mkoani humo.
Mhe. Rais Samia ameyasema hayo tarehe 17 Septemba 2023 alipokua Nachingwea mjini katika mkutano wa hadhara na wananchi na kuahidi kukomesha changamoto hiyo kama ilivyowasilishwa na Mbunge wa jimbo hilo, Mhe Amandus Chinguile (Mb).
“Migogoro baina ya wafugaji na wakulima changamoto hii tunaichukua na niwaahidi tutakwenda kukomesha kadhia hii ya wakulima kuuwawa kwa sababu ya wafugaji kutoa umuhimu zaidi kwa uhai wa n’gombe kuliko uhai wa mwanadamu hili tunakwenda kulikomesha,” amesema Mhe. Rais Samia.
Sambamba na hilo Mhe. Rais Samia amewahakikishia wakulima kuwa Serikali itashughulikia changamoto ya uvamizi wa wanyama wakali na waharibifu wanaopelekea kukwama kwa shughuli za uzalishaji na hata kupelekea vifo.
“Nasikitishwa sana kupata taarifa za Nachingwea kuwa kutoka mwaka 2021-2023 kiasi cha watu 10 hivi wameuwawa na wanyama wakali. Hii si sura inayopendeza hata kidogo na inaelekea hili jambo kwenye ngazi ya Wilaya na Mkoa limeshindikana kwa hiyo tunakwenda kukaa kikao cha Kitaifa tuone jinsi tunavyoweza kulishughulikia suala hili la wanyama, tunakwenda kulishughulikia ili mwende shambani mkalime kadiri Mungu anavyowajaali,” alisema Mhe. Rais Samia.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka wakulima wa Nachingwea kuongeza uzalishaji kupitia fursa ya pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali ili kuzidi na kuwa na Kilimo chenye tija kwa maendeleo ya nchi.