Morocco imekanusha habari ya safari ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuelekea mjini Rabat na kusema kuwa hakuna mpango wa kufanyika safari hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Morocco ilitupilia mbali madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa kwamba rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron atafanya ziara ya kuitembelea Morocco.
Afisa mmoja wa serikali ya Morocco ameliambia shirika la habari la nchi hiyo kwamba hakuna kibali kilichotolewa kwa Macron kusafiri kuelekea nchini humo.
Afisa huyu wa serikali ya Rabat ameongezea kwa kusema: “Ninashangaa waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa kutoa madai hayo ya upande mmoja na kujipa ruhusa ya kutoa tamko kama hilo.”
Siku chache zilizopita, Caterina Colonna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, alidai kuwa Rais Macron ataizuru Morocco hivi karibuni kwa mwaliko wa Mfalme wa nchi hiyo Mohammed wa VI.
Katika maelezo yake hayo, Colonna alikiri pia kuwepo mvutano kati ya Paris na Rabat.
Hivi karibuni, Morocco ilikataa hata kupokea msaada wa serikai ya Paris katika operesheni ya uokoaji ya tetemeko la ardhi na baada ya kukataliwa misaada hiyo ya Ufaransa na serikali ya Morocco, Macron alitoa video ya dakika mbili kwa Kifaransa ya kuwafariji watu wa Morocco.
Duru za kuaminika ziliripoti kuwa Mfalme wa Morocco hakujibu simu aliyopigiwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea hivi karibuni nchini humo.