Hayo yameelezwa na Taasisi ya Global Fund ambayo imebainisha kwamba, mabadiliko ya tabianchi na mizozo duniani vinakwamisha juhudi za kimataifa za kupambana na magonjwa matatu hatari ambayo ni Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu.
Ripoti ya taasisi hiyo ambayo ni mfuko wa kimataifa wa kupambana na maradhi hayo, inaonesha kwamba ijapokuwa miradi ya kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu imerejea kote duniani baada ya kuathiriwa na janga la virusi vya korona, lakini hivi sasa inakabiliwa na vizingiti vinavyotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mizozo.
Mkuu wa Taasisi ya Global Fund, Peter Sands, amesema majanga ya kimazingira mfano wa mafuriko yanaongeza idadi ya wagonjwa na hivyo kuwa vigumu matibabu kuwafikia.
Ongezeko la joto pia limefanya ugonjwa kama Malaria kusambaa hata kwenye maeneo ambayo kabla hayakukabiliwa na maradhi hayo. Afisa huyo amesema hali inayoendelea sasa inatishia malengo ya kutokomeza magonjwa hayo matatu ifikapo mwaka 2030.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, WHO inakadiria kuwa karibu watu milioni 250 wataambukizwa malaria mwaka huu. Watu milioni 247 waliambukizwa malaria mwaka 2021. Takriban nusu ya watu duniani wanaishi katika eneo ambalo liko hatarini na linaweza kuambukizwa malaria.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, kwa wastani bara la Afrika linarekodi kesi milioni 200 na vifo 400,000 kwa mwaka vinavyosababishwa na ugonjwa wa malaria.