Zaidi ya watoto 1,200 wamefariki katika kambi za wakimbizi nchini Sudan tangu mwezi Mei wakati huu pia watoto wachanga waliozaliwa wakikabiliwa na tishio na kufariki katika nchi hiyo inayokabiliwa na mapigano kufikia mwishoni mwa mwaka huu, imesema ripoti ya umoja wa mataifa.
Umoja wa mataifa pia umeeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya kiafya nchini haswa kwa watoto kutokana vita vinavyoendelea.
Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la UN lakushugulikia masilahi ya watoto la UNICEF, James Elder, inahofiwa kuwa watoto nchini Sudan watafariki kati ya sasa hadi mwishoni mwa mwaka.
Msemaji huyo wa UNICEF amesema kuwa watoto 333,000 wanatarajiwa kuzaliwa nchini Sudan kati ya mwezi Oktoba na Desemba.
Haya yanajiri wakati huu shirika la Umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi katika taarifa yake likieleza kuwa wafanyikazi wake katika jimbo la White Nile walikuwa wamesajili vifo vya zaidi ya watoto 1,200 kati ya tarehe 15 ya mwezi Mei na Septemba 14 katika kambi tisa za wakimbizi nchini Sudan.
Kambi hizo zilikuwa zinatoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka katika mataifa ya Sudan Kusini na Ethiopia.