Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa siku saba kwa Kampuni ya Chanzi Limited ambayo inajishughulisha na uzalishaji wa funza kwa ajili ya utengenezaji wa Chakula cha mifugo, kuhakikisha wanazuia harufu kali inayotokana na shughuli zinazofanyika kiwandani hapo.
Agizo hilo limetolewa Septemba 21, 2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria – NEMC Dkt. Thobias Mwesiga Richard alipofanya ziara katika eneo hilo la uzalishaji kufuatia agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo kutokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na tatizo hilo la harufu kali inayotoka katika eneo ambapo imekuwa ni kera kwa wananchi wa eneo hilo.
“Tumefanya ukaguzi katika eneo hili na tumejiridhisha kwamba kweli changamoto hiyo ipo, na changamoto yenyewe ni harufu kali inayotoka hapa ambayo inawaathiri wakazi wa maeneo haya na sisi maelekezo yetu kama Baraza ni kwamba kwanza kiwanda hiki kipo kwenye mchakato wa kuhamishiwa eneo lingine mbali na makazi ya watu na hapa tupo na Afisa Mazingira kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha na tumeongea na Mkurugenzi wa Jiji amesema wapo kwenye mchakato wa kukihamishia kiwanda hiki kwenye maeneo ambayo hakitakuwa karibu na wananchi” Amesema Dkt. Thobias.
“Nimuombe Mwekezaji afuatalie kwa haraka ili mchakato huo ukamilike mapema na Kwasababu mchakato huu utachukua muda kidogo kutokana na maandalizi ya miundombinu ya kiwanda, sisi kama Baraza tunatoa siku saba harufu hii iwe imedhibitiwa na isilete shida tena kwa wananchi kwakuwa ipo teknolojia mnayotumia kuzuia harufu hii kali na mbaya isiendelee kuathiri wananchi na baada ya hapo tukija tena tutawachukulia hatua ambayo ni kuwatoza faini pamoja na kukifunga kiwanda.” Amesisitiza Dkt. Thobias.
Kwa upande wa Mwekezaji wa eneo hilo Meneja wa Chanzi Limited Bi. Mayasa amesema wamepokea agizo hilo na watahakikisha wanadhibiti harufu hiyo isiweze kuleta kero tena kwa wananchi wa eneo hilo.