Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba,ametaja mambo matano ambayo Tanzania inajivunia kupitia mahusiano yake na China ikiwemo eneo la kuimarisha ulinzi na usalama.
Maeneo mengine, biashara na uwekezaji,kuboresha sekta ya afya,ujenzi wa miundombinu mikubwa barabara na reli ya Tazara, kidiplomasia na mahusiano baina ya watu na watu kutoka mataifa hayo mawili.
Hayo aliyabainisha Dar es Salaam juzi akiwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya sherehe ya kusherekea miaka 74 tangu kuanzishwa kwa Taifa la watu wa Jamuhuri ya China iliyofanyika katika ofisi za ubalozi huo ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wastaafu.
Akizungumzia kwenye eneo la ulinzi na usalama,alisema watumishi wa vyombo vya ulinzi wamekuwa wakienda nchini China kupata mafunzo mbalimbali ya kijeshi ambayo yamekuwa msaada katika usalama wa taifa.
“Ushirikiano wetu ulianza tangu kipindi tukiwa kwenye hali ngumu ya kiuchumi miaka ya 60 na wamekuwa wakitusaidia kuboresha jeshi letu la ulinzi na limeimarika kutokana na uhusiano uliopo,” alisema
Kuhusu eneo la biashara na uwekezaji alidai sekta hiyo imekuwa ikikua kwa kasi na China imekuwa moja kati ya nchi inayoongoza kwa kuleta mitaji mingi nchini.
“Mahusiano kati yetu na China tunajivunia ukaribu wetu kwa watu,maendeleo makubwa yaliyopatikana ikiwemo bomba la gesi kutoka mtwara, ujenzi wa Uwanja wa Taifa na ujenzi wa reli ya Tazara,” alisema