Serikali ya Guinea Conakry imewafuta kazi zaidi ya wanajeshi na maafisa 60 wa magereza kutokana na kashfa ya kutoroka jela rais wa utawala wa zamani wa kijeshi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, Moussa Dadis Camara na viongozi wengine watatu wa serikali yake ya zamani.
Makomandoo wenye silaha nzito walimtorosha jela Camara katika gereza la mji mkuu, Conakry, siku ya Jumamosi, lakini Camara na wenzake wawili walikamatwa tena na kurejeshwa gerezani siku hiyo hiyo baada ya kufanyika msako wa nchi nzima.
Kiongozi wa serikali ya kijeshi ya hivi ssa ya Guinea, Kanali Mamady Doumbouya amesema kuwa, amewafuta kazi wanajeshi na maafisa wa magereza kwa kutotekeleza ipasavyo majukumu yao na kwa utovu wa nidhamu.”
Wafungwa hao waliotoroka jela sasa wanakabiliwa na mashtaka mengine mapya baada ya kutoroka gerezani. Kabla ya hapo, viongozi hao wa utawala wa zamani wa kijeshi walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika vifo vya zaidi ya watu 150 na ubakaji wa zaidi ya wanawake 100 wakati wa maandamano ya 2009 jijini Conakry.