Kutumwa kama sehemu ya ujumbe unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wa maafisa zaidi ya elfu moja wa polisi wa Kenya nchini Haiti, iliotumbukia katika machafuko na ghasia, kutawezekana tu kwa ufadhili wa nchi wanachama wa shirika hilo la kimataifa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya amesema siku ya Alhamisi.
Kulingana na Waziri Kithure Kindiki, bajeti ya jumla ya kutumwa kwa maafisa wa polisi kwa mwaka mmoja, ambao wanalenga kurejesha utulivu katika nchi hii ya Karibea inayokumbwa na magenge yanayodhibiti mikoa yote ya nchi, inafikia dola milioni 600. “Isipokuwa rasilimali zote zitahamasishwa (…), wanajeshi wetu hawataondoka nchini,” ameiambia kamati ya bunge, akiomba fedha zitolewe na “nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa”.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinsha mwanzoni mwa mwezi Oktoba kwa ujumbe unaoongozwa na Kenya kusaidia polisi wa Haiti. Kenya imesema iko tayari kutoa hadi maafisa 1,000 wa polisi, na Kithure Kindiki amesema nchi kumi na moja pia zimejitolea kwa misheni hiyo, bila kuzitaja. “Hatupeleki jeshi kukalia maeneo ya Haiti, tunatuma jeshi kusaidia miundo ambayo tayari iko katika nchi hii kwa msingi wa ombi lao,” amehakikishia.
Mahakama ya Kenya mwezi Oktoba ilitoa agizo la kuzuia kutumwa kwa maafisa hao wa polisi hadi itakapotoa uamuzi juu ya ombi la kupinga kutumwa kwa maafisa hao. Uamuzi wa serikali ya Kenya kupeleka maafisa wa polisi nchini Haiti umeibua maswali na ukosoaji mwingi katika nchi hii ya Afrika Mashariki. Mahakama kuu ya Nairobi itazingatia rufaa iliyowasilishwa na wakili na mpinzani Ekuru Aukot, ambaye anadai kuwa kutumwa kwa maafisa hao ni kinyume cha katiba.