Wizara ya Elimu nchini Kenya imewaonya wakuu wa shule dhidi ya kuongeza ada kwa wanafunzi wa sekondari na sekondari ya juu nchini humo.
Waziri wa Wizara hiyo Ezekiel Machogu amesema ada kwa shule za bweni zitaendelea kudumu kama zilivyo sasa katika kiwango kilichokubaliwa na serikali.
Akizungumza katika Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Shule za Msingi uliofanyika katika Shule ya Msingi ya Sheikh Khalifa Bin Zayed mjini Mombasa jana, Bw. Machogu amesema serikali ya Kenya haina nia ya kuongeza ada kwa wanafunzi wa shule za sekondari na sekondari ya juu.
Mwezi uliopita, Shirikisho la Wakuu wa Shule za Sekondari za nchini Kenya walisema wataongeza ada kuanzia mwezi Januari, 2024 kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.