Mfanyabiashara wa jijini Tanga, Sultan Salim, amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuingilia kati mchakato wa upatikanaji wa mshindi wa zabuni wa eneo la Jamhuri Pack ‘Forodhani’ jijini humo.
Kauli hiyo imekuja baada ya mfanyabiashara huyo kudai amedhulumiwa haki yake kutokana na mchakato ulivyofanywa hadi kupatikana mshindi kuna taratibu na kanuni zimekiukwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Salim alisema kinachoonekana wanataka kumnyima haki yake kwa makusudi kwani alistahili kushinda tenda hiyo kutokana na dau kubwa alilotoa.
“Agosti Mosi, mwaka huu niliomba tenda hiyo ya Jamhuri Pack na nashukuru nilishinda kwakuwa dau langu la sh. milioni 2 na mia mbili hakuna ambaye alilifikia siku hiyo ya ufunguzi wa zabuni hiyo,” alisema na kuongeza;
“Lakini chakushangaza Halmashauri ya Jiji la Tanga ilivyofika Agosti 8, mwaka huu wakatoa makusudio ya upangaji na kumtangaza Ali Salim Mohamed kuwa mshindi kwa dau la sh. mil. 2.3 wakati siku ya ufunguzi tenda hiyo alitoa dau la sh. mil. 1.3 “.
Alisema anashangaa kuona mpinzani wake kutangazwa ameshinda tenda hiyo wakati siku ya ufunguzi alitoa dau dogo na yeye alitoa kubwa kitu ambacho kinampa maswali mengi bila majibu.
Akifafanua zaidi alisema baada ya sintofahamu hiyo aliandika barua kwenda halmashauri kupinga matokeo hayo pamoja na kuweka zuio lakini majibu yakabaki vile vile.
“Halmashauri ilijibu kwa kutilia mkazo matokeo yao ya awali waliyoyatoa na hata nilipoandika barua ya pili kwao na kuambatanisha na nyaraka zote za mchakato mzima ulivyoanza hadi kunionesha mimi ndiye nilipaswa kuwa mshindi, haikusaidia kitu kwani halmashauri ilikataa kupitia nyaraka zangu,” alisema Salim.
‘ kutokana na sintofahamu hiyo ndio maana ameamua kukimbilia kwa Waziri Mkuu, Majaliwa akiamini atalifanyia kazi na ukweli kuwekwa wazi’.