Wakati Zimbabwe ikipambana na mlipuko mbaya wa kipindupindu katika mji mkuu wake Harare, wagonjwa wanatibiwa huko Kuwadzana, ambapo ni kitovu cha janga hilo.
Siku ya Ijumaa, mamlaka ilitangaza hali ya hatari mjini Harare, jiji lenye watu milioni 1.5 ambapo vifo 13 vimeripotiwa kufikia sasa. Kote nchini, kumekuwa na vifo 150 na zaidi ya kesi 7,000 zinazoshukiwa za kipindupindu tangu kuzuka kwa ugonjwa huo kuanza mnamo Februari.
Nusu ya vifo katika mji mkuu vimetokea katika eneo lenye wakazi wengi la Kuwadzana, kulingana na waziri wa afya wa Zimbabwe Dk Douglas Mombeshora.
Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ni jambo linalotokea mara kwa mara katika miji ya nchi hiyo ambapo usambazaji wa maji safi na huduma za vyoo mara nyingi ni mdogo kutokana na miundombinu kuporomoka kutokana na kupuuzwa kwa miaka mingi.