Kongamano hilo la kitaifa lililowakutanisha washauri wa kitasnia wa vyuo mbali mbali vinavyonufaika na mradi wa HEET,lililenga kutoa elimu juu ya wajibu na umuhimu wa kamati hizi, kutokana na changamoto za ajira kwa wahitimu sokoni, na kuona namna kamati ya ushiriki wa kitasnia inavyoweza kuchangia uundaji mitaala itakayokidhi mahitaji ya soko pia kuwawezesha wahitimu kujiajiri.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mratibu wa Taifa wa Mradi wa HEET, Dkt. Kenneth Hosea alisema kamati hizi zinatarajiwa kuwa kiunganishi kwa watoa elimu na viwanda, ili kuhakikisha vyuo vinawandaa watalamu waliobobea, na wenye viwango vya juu ili kuendana na teknolojia sokoni.
Nae mratibu wa kamati ya ushauri kutoka wizara ya elimu, sayansi na teknolojia Dkt. Hadija Kweka alizitaka kamati hizi kushiriki kikamilifu katika kutoa ushauri wa kitaaluma katika tasnia zao hasa wakati wa uundaji na kutathmini mitaala, pamoja na kuhakikisha kamati hizo zinakua endelevu.
Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kimeshiriki kongamano hilo, ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya Kiuchumi(HEET) ambapo miradi mbali mbali inaendelea kutekelezwa ndani ya chuo hicho.