Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen, wamedai kuteka meli inayomilikwa na mfanyibiashara raia wa Israeli katika bahari ya Red Sea na wameipeleka pwani ya Yemen.
Tangazo hili limekuja siku chache baada ya wapiganaji hao kutishia kulenga mali zinazomilikiwa na Israeli katika bahari hiyo kutokana na vita vya na wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Msemaji wa Huthi Yahya Saree kupitia ukurasa wake wa X, zamani ukijulikana kama Twitter amethibitisha kutokea kwa kitendo hicho cha utekaji wa chombo hicho.
Mataifa ya Israel, Marekani na Japan yamelaani hatua ya wapiganaji hao kuteka meli hiyo.
Kwa mujibu wa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, chombo hicho kilikuwa kinamilikiwa na kampuni ya Uingereza na shughuli zake zilikuwa zinaendelezwa na kampuni ya nchini Japan.