Nyota wa kwenye ulimwengu wa soka duniani Lionel Messi sio mgeni kwenye kitendo cha kuvunja rekodi na anakaribia kuongeza nyingine kwenye orodha yake baada ya kutanganzwa kwa mnada wa Seti ya jezi sita alizotumia wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2022.
Kulingana na taarifa za Sotheby, mnada huu utafunguliwa rasmi kwanzia tarehe 30 Novemba, 2023 mpaka Decemba 14 jijini Newyork nchini Marekani ikitarajia zabuni kuwa zaidi ya dola milioni 10 ya jezi hizo zilizovaliwa na nahodha huyo wa Argentina wakati wa kila hatua ya mchuano wa Kombe la Dunia uliochukua mwezi mzima, ikijumuisha mechi ya fainali dhidi ya Ufaransa.
Zabuni hiyo ikifikiwa, bei ya seti ya jezi za Messi itapita jezi iliyovaliwa na staa wa mpira wa kikapu Michael Jordan katika Mchezo wa kwanza wa Fainali za ligi ya NBA ya mwaka 1998 kutoka kwenye msimu wake maarufu wa “the last dance”, ambayo iliuzwa kwa dola milioni 10.1 mwaka jana.
Jezi hiyo kwa sasa inashikilia rekodi ya dunia ya kuwa kitu chenye thamani zaidi kwenye safu ya kumbukumbu za michezo kuwahi kuuzwa kwenye mnada,” kulingana na jumba la mnada la Sotheby.
Kufikia hivi sasa, jezi iliyovaliwa na Messi yenye thamani kubwa zaidi iliuzwa kwa kiasi cha $450,000 (Tzs Bil 1.1) ikiwa ni jezi ambayo alivaa wakati wa mchuano wa El Clásico wa mwaka 2017 alipokuwa akichezea FC Barcelona dhidi ya Real Madrid ya Cristiano Ronaldo.
Bao lililofungwa na Messi kwenye dakika za mwisho lilikuwa goli lake la 500 kwenye maisha yake ya soka, ikipelekea ushindi wa mechi hiyo.