Wapelelezi nchini Kenya wanachunguza hali ya kiufundi ya gari alilokuwa akiendesha Kelvin Kiptum na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hazikimana waliokuwa na mtu mwingine wa tatu kabla ya kupata ajali mbaya ya barabarani kwenye barabara ya Eldoret Eldama Ravine Februari 11 2024.
Wapelelezi hao wanalichunguza gari aina ya Toyota Premio lenye nambari ya usajili KDL 566F alilokuwa akiendesha bingwa wa rikodi ya dunia Kelvin Kiptum kabla ya kupoteza udhibiti na kuondoka kutoka barabarani.
Wachunguzi hao wanasema bado ni mapema kueleza ni nini kilitokea kabla ya ajali hiyo iliogharimu maisha ya mwanaridha huyo aliekuwa na kocha wake raia wa Rwanda pamoja na mwanamke mmoja wakitokea Eldoret kuelekea Eldama Ravine.
Kiptum ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo huku kocha wake akiwa pembeni pamoja na mwanamke mwingine aliefahamika kama Sharon Chepkirui Jopkosgei.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi kaunti ya Elgeyo Marakakwet Peter Mulingi, Kelvin alipoteza udhibiti wa gari liliotoka barabarani na kwenda kujigonga kwenye mti umbali wa mita 60 kutoka barabarani.
Ripoti zinasema mwanadada aliyekuwa nyuma ya gari hilo alinusurika na anapatiwa matibabu.
Mbali na uchunguzi wa kiufundi, wapelelezi pia wanachunguza mwili wa mwanariadha huyo pamoja na kocha wake lakini pia kupata ushuhuda wa waliotokea katika êneo la tukio baada tu ya kutokea kwa ajali.