Mamlaka nchini Nigeria imethibitisha kuwa karibia wanafunzi 17 kutoka shule tofauti katika jimbo la Yobe Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo wamefariki baada ya kuambukizwa homa ya uti wa mgongo (Meningitis).
Miongoni mwa waliofariki ni wanafunzi wa shule za msingi na wengine katika shule za sekondari za bweni, kamishna wa elimu wa serikali, Mohammed Sani-Idris, aliambia BBC.
Jumla ya kesi 473 zinazoshukiwa zimerekodiwa hadi sasa, alisema. Homa ya uti wa mgongo ni maambukizi ambayo husababisha kuvimba kwa tabaka za nje za ubongo na uti wa mgongo.
Inaweza kuhatarisha maisha isipokuwa kutambuliwa na kutibiwa mapema.
Chanjo ni njia bora ya kuzuia ugonjwa wa uti wa mgongo.
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nigeria (NCDC) mapema mwakani kilitoa ushauri wa afya ya umma kuhusu ugonjwa huo.
Ilionyesha kuwa msimu wa kiangazi unaweza “kuongeza hatari ya kuambukizwa, hasa maeneo yenye msongamano yasiyo na hewa safi “.