Uhaba wa chanjo unakuja wakati kusini mwa Afrika ikipambana na mlipuko wa muda mrefu wa kipindupindu ambao umeua watu 700 nchini Zambia pekee.
Shirika la misaada la kimatibabu la Madaktari Wasio na Mipaka lilisema kuwa uhaba huo umeathiri timu zake zinazojaribu kukabiliana na milipuko katika zaidi ya nchi 16.
Wataalamu wa afya ya umma wamewataka watengenezaji kuharakisha utengenezaji wa chanjo hiyo ya kumeza. Dawa zote zinazozalishwa kwa sasa tayari zimehifadhiwa.
Mwezi Januari, Zambia ilianzisha kampeni iliyoungwa mkono na UNICEF kutoa chanjo dhidi ya kipindupindu kwa watu milioni 1.5. Mlipuko huo ambao ulianza mwaka 2023 sasa umeenea katika mikoa yote nchini, na kulazimu mamlaka kubadilisha uwanja kuwa kituo cha matibabu na kuchelewesha kufunguliwa kwa shule.
Kulingana na Save the Children, kesi za kipindupindu ziliongezeka mara nne nchini Malawi, Zimbabwe, na Msumbiji kutoka 2022 hadi 2023.