NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amekutana na kufanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Aidha, Kikao hicho kililenga kujadili maandalizi ya maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi zitakazofanyika mkoani Arusha, tarehe 1 Mei, 2024.
Katika kikao hicho Mhe. Katambi amewataka wajumbe wa kamati ya maandalizi kushirikiana kwa karibu ili waweze ili waweze kukamilisha shughuli walizopangiwa kwa wakati.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema maandalizi yanaendelea vizuri na kila kamati inafanya kazi kikamilifu ili kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafana.
Pia, Mhe. Makonda amewasihi wananchi wa mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ambapo mgeni rasmi wa
Maadhimisho hayo ya Sikukuu ya Wafanyakazi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwengine Mhe. Katambi ameuongoza ujumbe wa Mkoa wa Arusha na Viongozi wa TUCTA kukagua Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo sherehe za Mei Mosi zitafanyika.
Katika kikao hicho pia wameshiriki Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakioongozwa na rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, Wakuu wa Wilaya za mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Missaile Musa, Makamishna wa Kazi Wasaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zake.