Utendaji wa Wizara ya Maji na taasisi zake umeifanya kutambulika kimataifa ndani na nje ya bara la Afrika kwa kazi na utekelezaji wa miradi ya maji.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema makubwa yaliyoitambulisha Wizara ya Maji ni pamoja na Programu ya Lipa kwa Matokeo (P4R) ambapo Tanzania imekuwa mfano kati ya nchi zaidi ya 50 na kutambuliwa na Benki ya Dunia, hali ambayo inafanya Wizara ya Maji kuwa darasa kwa nchi nyingine duniani kuja Tanzania kujifunza utekelezaji wa miradi ya maji.
Haya yamewekwa wazi na Waziri Aweso (Mb) wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa katika Mkutano wa 15 (Mkutano wa Bajeti) wa Mwaka 2024/2025 Bungeni Jijini Dodoma.
Bajeti hiyo imesheheni masuala mapya ikiwamo kuanza kutumia teknolojia ya matumizi ya Dira za maji za malipo kabla (pre-paid water meters) badala ya Dira za kulipa baada ya matumizi (post-paid water meters) ili kuhakikisha uendelevu wa huduma ya maji vijijini na mijini.
Ameainisha jingine kubwa ni kupatikana kwa chanzo kipya cha fedha za utekelezaji wa miradi ya maji kupitia Hatifungani ambapo Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga imekuwa ya kwanza kuzindua uuzaji wa Hatifungani ya Kijani yenye thamani ya Shilingi bilioni 53.12.
Akizungumzia vipaumbele vya Wizara ya Maji, Waziri Aweso amesema ni pamoja na kuimarisha matumizi ya mitambo ya uchimbaji wa visima na mabwawa ili kufikisha huduma kwenye vijiji ambavyo havina huduma pamoja na kutekeleza Programu ya kuchimba visima 900 kwa maana ya kila jimbo la uchaguzi kupata visima vitano, na ujenzi wa mabwawa madogo madogo.
“Wizara imeweka vipaumbele ambavyo vitazingatiwa katika mpango na bajeti ya mwaka 2024/25 ili kufikia lengo la kuwapatia huduma ya majisafi na salama kwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa mijini,” Waziri Aweso amesema.