Ajali mbaya imetokea Nchini Haiti baada ya Lori la kubeba Mafuta kuanguka na kulipuka, na kusababisha vifo vya Watu zaidi ya 15 huku wengine 40 wakiwa wamejeruhiwa vibaya.
Ajali hiyo ilitokea Jumamosi, Septemba 14, katika Mji wa Bandari wa Miragoane, ulioko kusini mwa Nchi hiyo na mmoja wa waliojeruhiwa vibaya alisafirishwa kwa Helikopta ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya matibabu ya dharura.
Aidha Waziri Mkuu wa Haiti, Garry Conille, alitembelea eneo la tukio na kutoa pole kwa wahanga wa ajali hiyo huku akizungumza akiwa kwenye helikopta katika mji mkuu wa Port-au-Prince, alisema, “Ni tukio la kusikitisha sana, tumeshuhudia maafa makubwa, watu wengi wamejeruhiwa na kuungua vibaya.”
Waathiriwa wengine wa mlipuko huo walisafirishwa hadi Hospitali ya Saint Boniface, mashariki mwa Les Cayes, kwa ajili ya matibabu zaidi, na kulingana na vyombo vya habari vya ndani, mlipuko huo ulitokea wakati Waathiriwa walipokuwa wakikusanya Mafuta kutoka kwenye Lori hilo lililopinduka.
Haiti, Taifa lenye Watu takriban Milioni 12, limekuwa likikabiliwa na uhaba mkubwa wa Mafuta, hali inayochangiwa na mapigano ya magenge yanayovuruga uingizaji wa bidhaa Nchini humo, na hivyo kuongeza changamoto kwa Raia wake.