Viongozi wa dini na wanasiasa wametoa shukrani kwa juhudi za viongozi wa mkoa wa Tanga pamoja na wananchi katika kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 unakuwa wa haki na salama bila vurugu.
Kauli hizo wamezitoa Leo viongozi wa dini pamoja na vyama vya siasa wakati wakizungumza na waandishi wa Habari juu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 ulivyofanyika.
Sheikh wa Mkoa wa Tanga Juma Luhwuchu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Tanga, alieleza kwamba sala na dua zilizofanywa na viongozi wa dini, waislamu na wakristo, zilichangia kudumisha amani. Aidha, alitoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa, Balozi Dkt. Batilda Burian, kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na utulivu.
Naye Mchungaji Haule Haule, Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Tanga, aliongeza kuwa uwazi uliokuwepo kuanzia hatua za uandikishaji hadi kufanyika kwa uchaguzi ulisaidia kudumisha amani na kutoa shukrani kwa Mungu na kwa viongozi wote waliofanikisha hali hiyo
Kwa upande wa Kauli za viongozi wa vyama vya siasa wakiongozwa na Ramadhani Manyeko, Naibu Kamishna wa Chama cha NCCR Mageuzi Mkoa wa Tanga, alieleza kuridhika na namna ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilivyoshirikiana na vyama vyote katika mchakato wa uandikishaji na uchaguzi.
Pia Rashid Amir ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha TLP Mkoa wa Tanga, alisifu demokrasia iliyoonyeshwa wakati wa uchaguzi, akimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuweka mazingira bora yaliyohakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na upendo.
Kauli hizi zinadhihirisha mshikamano uliopo kati ya viongozi wa dini, wanasiasa, na wananchi katika kuhakikisha maendeleo ya demokrasia na amani ya nchi.