NAIBU Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya ametoa wito kwa wabunifu, wahandisi, na wadau wote wa Sekta ya Ujenzi kuhakikisha kila mradi wa ujenzi unazingatia masuala ya uhifadhi wa mazingira, kupunguza taka zinazozalishwa na kuongeza ufanisi wa rasilimali.
Kasekenya ametoa wito huo katika hafla ya Tuzo za Ujenzi na Majengo ya Afrika Mashariki zilizofanyika Dar es Salaam na kubebwa na kauli mbiu “Kuzingatia Mabadiliko ya Kidijitali katika Sekta ya Ujenzi” na kuangazia maendeleo ya Sekta ya Majengo kupitia teknolojia na ubunifu.
Ameeleza kuwa katika nchi za Afrika Mashariki ni wakati muafaka wa kuwekeza katika miradi inayozingatia uendelevu na yenye athari ndogo kwa mazingira kwa kuhusisha matumizi ya vifaa vya kijani, nishati safi na ubunifu wa majengo yanayoweza kuhimili hali mbalimbali za hewa.
“Niwahakikishie kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kuhamasisha ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa katika Sekta ya Ujenzi kupitia Sera na Programu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa dhana ya ujenzi endelevu inatekelezwa kikamilifu”, ameeleza Eng. Kasekenya.
Eng. Kasekenya amebainisha kuwa tuzo hizo za ujenzi na majengo za Afrika Mashariki zinalenga kuongeza ushindani miongoni mwa wadau wa Sekta ya Ujenzi pamoja na kuwa chachu ya utoaji wa huduma bora.
Vilevile, Eng. Kasekenya amewapongeza waandaaji wa tuzo hizo kwa juhudi zao katika kuleta pamoja wadau wa Sekta ya Ujenzi ili kutambua na kuhamasisha uvumbuzi na ufanisi katika sekta hiyo.