Mahakama ya Wilaya ya Kigoma Mkoani Kigoma imehuhukumu kwenda jela miaka 30 Afisa ustawi wa jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Frank Mabuga baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike wa miaka 13.
Hukumu hiyo imesomwa kwa takribani dakika 29 katika chumba cha siri (in camera) mbele ya hakimu mkazi mwandamizi Eva Mushi.
Shauri hili lilitajwa kwa mara ya kwanza Februari 22 mwaka jana 2022 mbele ya Hakimu wa wilaya Venance Mwakitalu ambapo Frank alituhumiwa kumbaka mara mbili usiku kucha katika nyumba ya kulala wageni ya Ishimwe mnamo Desemba 19, 2021 nakumsababishia maumivu makali na michubuko sehemu za siri.
Muathiriwa wa ubakaji huo ni mtoto wa kike miaka 13 ambaye alikuwa mkazi wa mtaa wa Mlole.
Shauri hili lilikuwa na mashahidi sita upande wa Jamuhuri na vielelezo viwili huku hii leo upande wa mshitakwia alikuwepo wakili Ignatus Rweyemamu ambaye hata hivyo hakutaka kuzungumza chochote mara baada ya hukumu.
Hakimu mushi amefafanuwa kuwa hukumu hii ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 130 kifungu kidogo (1) (2) e na kifungu 131 kifungu kidogo cha kwanza cha kanuni ya adhabu namba 16 cha 2019 na marekebisho yake ya mwaka 2022 na akamuhukumu kwenda jela miaka 30.
Wakili wa serikali Happiness Mayunga ameeleza kuridhishwa na hukumu hiyo na kwamba ni vema watu waliopewa wadhama ya kulinda mtoto wawe mfano bora badala ya kuwa mstari wa mbele kuvunja sheria.