Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) kimetangaza mipango ya kuhamasisha msaada wa haraka wa kuisaidia Tanzania kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Marburg.
Katika taarifa yake, Afrika CDC imethibitisha kutumwa timu ya wataalamu 12 wa afya ya umma hapa nchini .
Hatua hiyo ya Afrika CDC imekuja baada ya Tanzania kutangaza kuzuka mlipuko wa ugonjwa huo katika mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kesi moja ya ugonjwa huo imethibitishwa na kuna kesi nyingine 25 zinazoshukiwa ni za ugonjwa huo.
Timu hiyo inajumuisha wataalamu wa magonjwa, wataalamu wa mawasiliano katika mazingira ya hatari na wataalamu wa kuzuia maambukizi, udhibiti na uchunguzi wa maabara.
Dhamira yao ni kusaidia uchunguzi na utafiti na pia kusimamia kesi nakushirikishwa jamii ili kuzuia kuenea ugonjwa huo wa kuambukiza na ambao mara nyingi huwa mbaya.