Mtu mmoja Nchini China, aliyekuwa na hasira kuhusu makubaliano ya talaka, anashikiliwa na Polisi baada ya kugonga umati wa watu kwa Gari waliokuwa wakifanya mazoezi katika Kiwanja cha michezo kilichopo Zhuhai, kusini mwa China na kusababisha vifo vya Watu 35 huku wengine wengi wakijeruhiwa vibaya.
Polisi walimkamata Mtu huyo mwenye umri wa miaka 62, ambaye alikimbizwa Hospitali kwa matibabu ya majeraha yanayohusishwa na jaribio la kujiumiza mwenyewe.
Inaelezwa kuwa Mtuhumiwa alikuwa na hasira kubwa kuhusu mgawanyo wa mali katika talaka yake na Polisi wamesema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa alifanya shambulizi hili kama njia ya kulipiza kisasi.
Video za tukio hilo zilienea kwenye mitandao ya kijamii, hasa kwenye jukwaa la X, ambapo Watu waliweza kuona majeruhi wakiwa wamelala kwenye Uwanja huku huduma za dharura zikitolewa na Katika video moja Mtu mmoja anasema “mguu wangu umevunjika”.
Tukio hili linakuja ikiwa ni moja ya matukio ya shambulio kwa Raia Nchini China, ambapo wazo la kulipiza kisasi kwa kutumia nguvu limeonekana mara kadhaa, kama ilivyoshuhudiwa katika matukio mengine ya kigaidi ambayo yalitokea mwaka huu Kwa mfano, Oktoba, Mtu mwingine alikamatwa kwa mashambulizi ya kisu kwenye shule moja huko Beijing, huku mwezi Mei shambulizi jingine likitokea hospitali moja huko Yunnan.
Rais Xi Jinping alitoa kauli akisisitiza kuwa Mtuhumiwa anapaswa kuadhibiwa kwa sheria na akatoa wito kwa Serikali za mitaa kuongeza juhudi za kudhibiti migogoro kabla ya kutokea, ili kuepuka matukio ya vurugu kama haya.