Idadi ya Watu waliofariki katika ajali iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni Kibaoni Jijini Arusha ikihusisha lori na magari mengine madogo matatu imeongezeka na kufikia Watu 25 huku majeruhi wakiwa ni 21.
Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP Awadhi Juma Haji amesema hayo alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru ambapo amesema ajali hiyo imetokea jana February 24,2024 muda wa saa 11:00 jioni katika Barabara ya Arusha Namanga.
CP Awadhi amesema waliofariki katika ajali hiyo ni Wanaume 14 Wanawake 10 na Mtoto mmoja wa kike ambao jumla yao ni 25 huku akiitaja idadi ya Raia wa kigeni waliofariki kuwa ni 7.
Awadhi amesema majeruhi ni 21 na kati yao Wanaume ni 14 na Wanawake ni 7 na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni kufeli breki ya lori kitendo kilichopelekea lori hilo kuyagonga magari mengine yaliyokuwa mbele yake na Polisi wanaendelea kumtafuta Dereva aliyesababisha ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.