Mwanaume mmoja kutoka Michigan Nchini Marekani amekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya jaribio la mauaji kwa kukusudia baada ya kusafiri zaidi ya kilomita 1,000 kwenda Pennsylvania na kuchoma moto nyumba ya Mwanaume aliyekuwa akizungumza na mpenzi wake wa zamani.
Kwa mujibu wa ripoti za Polisi moto huo ulitokea majira ya saa 11 alfajiri ambapo Wakaazi sita waliokuwemo ndani waliweza kujiokoa baadhi yao wakiruka kupitia madirisha ya ghorofa ya pili huku mbwa wawili wakipoteza maisha kwenye moto huo.
Uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa moto huo ulianzishwa kwa makusudi na kupitia Kamera za usalama zilimuonyesha Mshukiwa akifika katika eneo hilo kwa Gari aina ya Volkswagen Passat yenye namba za usajili za Michigan akishuka na kitu mikononi na dakika 15 baadaye moto mkubwa ulilipuka mara baada ya yeye kuondoka.
Kwa kutumia teknolojia ya kusoma namba za Magari na kamera za mitaa Polisi walimfuatilia mshukiwa hadi Michigan ambapo walimkamata na kumkuta na vidhibiti kama vifaa vya kufungua kufuli, simu, kompyuta na majeraha ya moto mikononi mwake na hivi sasa uchunguzi unaendelea kubaini sababu zaidi za tukio hilo.