Waziri mkuu wa Albania ametangaza kuwa serikali inakusudia kuzuia ufikiaji wa TikTok kwa mwaka mmoja baada ya mauaji ya mvulana wa shule mwezi uliopita kuibua hofu kuhusu ushawishi wa mitandao ya kijamii kwa watoto.
Akizungumza Jumamosi Edi Rama alitangaza marufuku iliyopendekezwa itaanza Januari.
TikTok ilisema inatafuta ufafanuzi wa haraka kutoka kwa serikali ya Albania kuhusu marufuku iliyopendekezwa.
Kulingana na taarifa ushahidi bado haujapatikana kwamba mtu aliyedaiwa kumdunga kisu mvulana wa miaka 14, au mwathiriwa mwenyewe, alikuwa na akaunti za TikTok.
Wakati wa mkutano katika mji mkuu wa Albania wa Tirana na walimu, wazazi na wanasaikolojia Rama alitaja TikTok kama “jambazi wa ujirani”.
“Tunaenda kuifunga kwa mwaka mmoja na tutaanza kusambaza programu ambazo zitahudumia elimu ya wanafunzi na kusaidia wazazi kufuata safari ya watoto wao,” Rama alisema.