Katika kusheherekea siku yake kuzaliwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan (63) ametoa sadaka kwa vituo vya kulelea Watoto Yatima ikiwemo Msimbazi Center huku wito ukitolewa jamii kupinga vitendo vya ukatili.
Akimuwakilisha Rais Dr.Samia, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema:
“Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan nipo hapa kukabidhi sadaka kwa ajili ya Kituo cha Watoto Yatima Msimbazi wanaoishi katika mazingira magumu kinachosimamiwa katika Kanisa Katoliki”.
“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais tunasema shukrani nyingi na tunashukuru uongozi wa Kanisa, leo ni siku maalum kwa Mheshimiwa Rais wetu Dr.Samia Suluhu Hassan ametimiza umri wa miaka 63 na katika furaha na bashasha yake ameona ashiriki katika kumtukuza na kumshuruku Mwenyezi Mungu na kutoa kwake ameamua kwa makusudi kutoa katika vituo vya watoto yatima miongoni mwa vituo ameamua kutoa katika Kituo cha Msimbazi Center na Mburahati,”
“Tunaomba Watanzania wote lakini viongozi wa Dini tuendelee kumuombea Rais Samia aendelee kuliongoza taifa letu kwa mafanikio makubwa ambayo kwa hakika tumeyaona ndani ya muda ambao yeye ameliongoza taifa, tumeshuhudia mambo makubwa ikiwemo uboreshwaji wa huduma za kijamii upande wa elimu, afya na shughuli za Kiuchumi tumuombee heri nyingi aendelee kulitunza na kuliongoza taifa hili,”
“Na kama unaona anafanya mambo kwa mifano nyakati zimekuwa ngumu wapo watu wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, wakina Mama Rais ni mpenzi wa watu wote ikiwemo watoto na wakina mama, na ndio maana kwa kufanya hivi leo anathibitisha mapenzi yake kwa watoto anawatakia heri nyingi sana,”. Amesema Naibu Waziri Ulega.