Mshtakiwa Salim Fadhil(31) aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya wizi wa viatu vyenye thamani ya Shilingi Elfu Sitini (60,000) ameachiwa huru katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo baada ya mlalamikaji katika kesi hiyo kushindwa kufika mahakamani.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi, Claudis Kipande wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa mara ya kwanza kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa makosa yake.
Baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka yanayomkabili alikana kutenda kosa hilo na kudai kuwa amesingiziwa na mlalamikaji ambaye ni Arafat Salum, kwani yeye anafanya biashara ya kuuza viatu.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Kipande alisema kwa kuwa mlalamikaji ameshindwa kufika Mahakamani hapo ili kesi iendelee basi anaifuta.
“Mlalamikaji ameshindwa kufika Mahakamani ili tusikilize ushahidi wake, hivyo ninaiondoa kesi hii na wewe mshtakiwa kama kweli ni mwizi utakamatwa tena na utaletwa hapa,” alisema Hakimu Kipande.
Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 17, 2024 katika mtaa wa ushiri Wilaya ya Ilala, ambapo aliiba viatu jozi tatu zenye thamani ya sh. 60,000, mali ya Salum Arafat.