Gavana wa zamani wa benki kuu ya Nigeria Godwin Emefiele alishtakiwa kwa kuchapisha noti mpya kinyume cha sheria na kutoa mabilioni ya naira bila idhini ya rais na kukiuka sheria zilizowekwa.
Emefiele, ambaye tayari anakabiliwa na kesi tofauti ya ulaghai, alikana mashtaka mapya wakati wa kufikishwa mahakamani siku ya Jumatano katika mahakama ya Abuja. Aliachiliwa kwa dhamana.
Waendesha mashtaka wa serikali wanasema kati ya Oktoba 2022 na Machi 2023, Emefiele aliamuru kuchapishwa kwa noti mpya za naira 1,000, 500 na 200 bila idhini ya rais na bodi ya Benki Kuu ya Nigeria.
Uchapishaji wa noti mpya ulikusudiwa kupunguza matumizi ya pesa taslimu katika uchumi lakini badala yake ulitatiza biashara na kusababisha hali ngumu kwa raia huku Nigeria ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais wa mwaka jana ambao Bola Tinubu alishinda