Mwanamke mmoja wa Florida aitwaye Sarah Boone hatimaye amehukumiwa kwenda jela maisha kwa Kumuua Mpenzi wake kwa kumfungia kwenye sanduku la nguo kwa masaa kadhaa hadi kufa, Jaji wa Mahakama ya Jimbo la Florida, Michael Kraynick ameamua.
Boone, mwenye umri wa miaka 47, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumuua Mpenzi wake aitwaye Jorge Torres Jr. kwa kumfungia kwenye begi la nguo kwa masaa kadhaa hali ambayo ilisababisha kifo chake.
Mwanamke huyo amekiri kumuingiza Torres kwenye begi na kumwacha akiwa ndani yake kwa usiku mzima baada ya kurekodi video iliyokua ikionyesha Mwanaume huyo akipiga kelele na kuomba msaada wa kutolewa ndani ya begi hilo lililokua ndani kwao.
Baada ya tukio hilo Boone alijitetea na kusema kwamba alikuwa anateswa na Torres kwa muda mrefu na kudai kuwa aliathirika kisaikolojia hali iliyosababisha afanye maamuzi aliyofanya ya kumfungia katika begi la nguo na kumtelekeza Mpenzi wake hadi kifo.
Kisa hicho kilitokea Februari ya mwaka 2020 wakati wawili hao walikuwa wakicheka na kucheza mchezo wa kujificha, inasenekana kuwa Torres alijitolea kuingia katika begi hilo lakini baada ya kufanya hivyo Boone alimfungia na kumuacha bila msaada.
Katika maamuzi ya mwisho ya kesi hiyo, Jaji Michael Kraynick alikataa ombi la Mtuhumiwa kabla ya hukumu, akizingatia ushahidi wa kesi na uamuzi wa awali wa Mahakama, Boone amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumuua Torres kwa njia hiyo ya kikatili.