Michael Sullivan Raia wa Marekani amepata fidia ya dola milioni 13( billioni 34 za kitanzania) baada ya kutumikia kifungo cha miaka 27 gerezani kwa kosa ambalo hakuwa ametenda ambapo alifungwa mwaka 1987 kwa madai ya kumuua Wilfred McGrath lakini teknolojia mpya ya DNA ilithibitisha kuwa ushahidi uliomtia hatiani haukuwa sahihi na mnamo mwaka 2013 Sullivan aliachiliwa huru baada ya kesi yake kusikilizwa upya.
Maisha ya Sullivan Gerezani yalikuwa magumu ambapo alipoteza Mama yake na ndugu wanne wakati yupo Gerezani lkini pia alikumbana na mashambulizi kadhaa akiwa Gerezani yaliyomsababishia majeraha makubwa.
Hata hivyo licha ya fidia hiyo kubwa aliyopewa na Mahakama sheria za Jimbo la Massachusetts zinapunguza malipo kwa kesi za makosa ya uhalifu usio wa haki (wrongful convictions) hadi dola milioni 1 ( bilioni 2 za kitanzania) na kumfanya Sullivan kutokupokea fidia yote kwa wakati mmoja, jambo ambalo limeibua mjadala kwa Watu wanaoamini kuwa Sheria hiyo haijali uzito wa madhara aliyoyapata Mtu aliyetiwa hatiani kimakosa hasa ikizingatiwa kwamba fidia ya dola milioni moja inaweza kuwa ndogo kulinganisha na mateso na upotevu wa muda wa miaka mingi Gerezani.
Hivi sasa, Sullivan anaishi na dada yake huku akikabiliana na changamoto za kurejea katika maisha ya kawaida kutokana na athari alizozipata akiwa Gerezani.
Sullivan amepanga kutumia sehemu ya fidia yake kusaidia Vizazi vijavyo vya Familia yake “Ingawa pesa haziwezi kurejesha miaka niliyopoteza, natumaini zitatoa mustakabali mzuri kwa familia yangu” alisema.