Taasisi za Serikali, Asasi za kiraia pamoja na wananchi wameendelea kukumbushwa kuwasilisha mapendekezo yao ya maboresho mbalimbali ya sheria katika Tume ya Kurekebisha Sheria kwa ajili ya kufanyiwa utafiti.
Rai hiyo imetolewa jana Jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Griffin Mwakapeje alipokutana na Jumuiya ya Asasi za kirai zinazoratibiwa na Taasisi ya mafunzo ya MSTCDC walipotembelea ofisini za tume hiyo jijini Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha maoni na mapendekezo yao ya maeneo mbalimbali yenye changamoto za kisheria.
“Tume ndiyo chombo pekee cha kisheria ambacho kimewekwa na Bunge kwa ajili ya kuisaidia serikali kufanya mapitio na kuangalia changamoto mbalimbali za kisheria na kuzifanyia utafiti.
Na utafiti ambao sisi tunaufanya tunahusisha jamii ili mwisho wa siku sheria inapokuja kutungwa wote tunakuwa kwenye uelewa mmoja,” amefafanua Mwakapeje.
Ameongeza kuwa sheria zikifanyiwa utafiti zinaweza kuishi miaka mingi zaidi badala ya kubadilishwa mara kwa mara.
Akizungumzia kuhusu kikao cha Tume hiyo na Jumuiya hiyo ya Asasi za Kirai, Mwakapeje amesema jumuiya hiyo ilifanya utafiti kwenye mbalimbali ambazo ni pamoja na sheria za jinai, sheria za jinai na masuala ya uraia, masuala ya kikatiba, sheria za kimataifa na sheria za vyombo vya habari na upatikanaji wa taarifa.
“Baada ya utafiti wao waliona ni sahihi kuja kutushirikisha tafiti zao walizofanya kwa kujua kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria ndiyo chombo pekee ambacho kinafanya utafiti na mapitio ya sheria zote na hivyo wakaona waje watushirikishe mapendekezo yao ili na sisi tuweze kufanya utafiti na kuishauri serikali,” alisema Mwakapeje.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (mstaafu) January Msoffe ameipongeza jumuiya hiyo na kuwaahidi ushirikiano zaidi huku akitoa wito kwa wadau wengine kuweza kutoa mapendekezo yao ya maboresho ya sheria mbalimbali ili kuweza kuwa na sheria bora zaidi.
Kiongozi wa msafara wa jumuiya hiyo ya asasi za kiraia ambaye pia ni rais wa chama cha Mawakili (TLS), Wakili Harold Sungusia ameipongeza Tume kwa kazi wanazofanya za utafiti wa sheria mbalimbali na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi kwa kutoa mapendekezo katika maeneo mbalimbali hasa katika mchakato wa Katiba unaoendelea.