Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Fredrick Shoo ameiomba Serikali kukataa na kukemea kwa nguvu yote wale wote wanaoonesha dalili za kuwagawa Watu kwa utofauti wa Dini na kusema hata pale Mtu anaposema jambo la kuipendeza Serikali iwapo amejenga hoja yake katika msingi wa kuwagawa Watu kidini au kwasababu nyingine yoyote akemewe kwakuwa hana nia njema.
Dkt. Shoo amesema hayo mbele ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika Chuo cha Tumaini Makumira, Arusha leo August 21,2023.
Dkt. Shoo amenukuliwa akisema “Umoja wa Taifa letu la Tanzania, mshikamano ni muhimu kuliko Mtu au kundi lolote, niwaombe Viongozi wenzangu wa Dini zote, niwaombe Wanasiasa, kuacha kabisa kujaribu kuwagawa Watu kwa misingi ya Dini au kwa misingi ya itikadi iwayo yoyote ya kisiasa na kwa misingi ya maslahi binafsi”
“Niombe Serikali yako kukataa na kukemea kwa nguvu yote wale wote wanaoonesha dalili za kutugawa kwa utofauti wa Dini zetu, hata pale Mtu anaposema jambo la kuipendeza Serikali iwapo amejenga hoja yake katika msingi wa kutugawa kidini au kwasababu nyingine yoyote huyo akemewe, tumkatae hana nia njema”