Ni Waziri wa Nishati, January Makamba ambae amesema Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere umefikia asilimia 67 na kubaki asilimia 33 tu toka Ujenzi huo uanze na kusema kazi iliyokuwa ikifanyika kwa miaka miwili na nusu.
Hivi sasa imefanyika ndani ya mwaka mmoja hadi kufikia asilimia hizo. Alisema Disemba 2018 hadi Juni 2021 mradi uliyoanza (miaka miwili na nusu) kazi ilifika asilimia 37, lakini kuanzia Juni 2021 hadi Julai mwaka huu, kazi imefanyika kwa asilimia 30.
Makamba alieleza hayo juzi, mbele ya wajumbe wa bodi ya Tanesco, Wahariri na Wanahabari wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea mradi huo kujionea hatua iliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja.
Katika ziara hiyo wahariri na wanahabari walipata fursa ya kujionea maeneo nane muhimu katika mradi huo ikiwemo:
> Tuta kuu (main dam): ujenzi Juni 2021 ulikua 26%, sasa hivi 78%.
> Daraja la kudumu (permanent bridge): Juni 2021 ulikuwa 37.8%, sasa hivi 95%.
> Njia za maji kuendesha mitambo (power water ways ): Juni 2021 ulikuwa 43%, sasa hivi 85%.
> Kituo cha kusafirishia umeme (switchyard): Juni 2021 kilikua 38%, sasa hivi 89.7%.
Akiongea kwa niaba ya wahariri na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa hatua kubwa katika mradi huo.
“Tulikuwa tunasikia tu mradi unaendelea lakini hatukuwa na taarifa sahihi. Tumeona, tunashukuru na tunapongeza hatua iliyofikiwa.” amesema Balile