Afisa wa Polisi wa Kitengo (DPO) makao makuu ya polisi huko Bompai, Kano nchini Nigeria, Daniel Amah, ametunukiwa Tuzo ya Uadilifu katika Utumishi wa Umma na Rais Muhammadu Buhari.
Amah, mzaliwa wa Jimbo la Plateau, alikataa kiasi cha hongo ya dola 200,000 (Sh milioni 466.4) ili aweze kumaliza kesi inayomhusisha opereta wa duka la kubadili fedha za kigeni (Bureau de Change), Ali Zaki, ambaye alikula njama pamoja na wengine kumuibia Mnigeria mmoja zaidi ya dola 750,000.
Afisa huyo wa polisi hakukataa tu hongo hiyo bali pia alihakikisha kwamba mshukiwa amefikishwa mahakamani.
Buhari alimtunuku Amah, Mrakibu wa Polisi (SP), katika mkutano wa nne wa kilele wa kitaifa kuhusu kupunguza vitendo vya rushwa katika sekta ya umma, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ikulu, Abuja.
Mkutano huo wa siku moja wa kupinga rushwa, wenye kaulimbiu, “Rushwa na sekta ya elimu”, umeandaliwa na Taasisi Huru ya Kuzuia Rushwa na Makosa Mengine Yanayohusiana Nayo (ICPC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu wa Serikali ya Shirikisho (OSGF) na Bodi ya Pamoja ya Udahili na Masomo (JAMB).
Akikabidhi tuzo hiyo kwa SP Amah kwa kuonyesha ujasiri na uadilifu wa kipekee katika utekelezaji wa majukumu yake, Rais Buhari alimpongeza mshindi huyo kwa tabia yake bora katika kutekeleza wajibu wake.
Rais alitoa wito kwa Wanigeria wanaoshikilia ofisi za umma kuiga tabia ya kupigiwa mfano ya mshindani huyo kwa nia ya kupambana na ufisadi nchini humo.
Kulingana na Buhari, “Tunahitaji kumaliza ufisadi ili Nigeria isonge mbele.”