Wizara ya Malisili na Utalii imesema endapo mtumishi wa Wakala ya Huduma za Misitu (TFS) au wa Jeshi la Uhifadhi atabainika kukiuka masharti ya kazi na kama atakuwa ametenda kosa la kijinai na pia kinidhamu watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) wakati akijibu swali la Mhe. Seif Khamis Said Gulamali(Mb) aliyetaka kujua Je, ni adhabu gani inatolewa kwa watumishi wa TFS wanaobainika kudhuru raia na mali zao.
Aidha Mhe. Kitandula aliongeza kuwa kwa upande wa kinidhamu Mwajiri atamfungulia mashtaka kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma zikisomwa pamoja na kifungu 9 (3) cha Amri za Jeshi la Uhifadhi za mwaka 2022.
”Pindi mtumishi huyo akikutwa na hatia, anaweza kufukuzwa kazi, kupunguziwa mshahara au kushushwa cheo na mshahara” aliongeza Mhe. Kitandula.
Mhe. Kitandula alikazia kuwa Sheria ya Misitu Sura 323 imeweka makatazo ambayo mtu yeyote anayekiuka anakuwa ametenda makosa ya jinai na hivyo, kulazimika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, Katika utekelezaji wa majukumu hayo Watumishi wanatakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na misingi ya haki za binadamu.