Serikali ya Australia imewasilisha muswada wa sheria Bungeni unaopendekeza kupiga marufuku Watoto chini ya miaka 16 kutumia Mitandao ya kijamii na Kampuni zitakazokiuka sheria hii zitakabiliwa na faini ya hadi dola milioni 32 za Marekani (bilioni 84 TZS).
Sheria hii inalenga kuanzisha mfumo wa kuthibitisha umri kwa kutumia biometriki au vitambulisho vya Serikali ili kuhakikisha Watoto hawafungui akaunti na hakutakuwa na nafasi ya ruhusa ya Wazazi wala msamaha kwa akaunti zilizopo tayari.
Watoto bado wataweza kutumia huduma kama ujumbe wa moja kwa moja, michezo ya mtandaoni, na majukwaa ya afya ya akili kama Headspace huku Serikali ya Nchi hiyo ikisema hatua hii inalenga kulinda Watoto dhidi ya maudhui yenye madhara, ikiwemo yaliyohamasisha matumizi ya dawa za kulevya, kujidhuru, na picha zenye madhara.
Sheria hii pia itawalazimisha Wamiliki wa mitandao kuhakikisha faragha za watumiaji kwa kufuta taarifa zinazokusanywa mara baada ya matumizi.