Moja ya habari iliyokamata headlines mwanzoni mwa wiki hii ni pamoja na mpishi kutokea nchini Nigeria, Hilda Bassey Effiong, almaarufu kama Hilda Buci kuvunja rekodi ya dunia ya Guinness ya kupika kwa muda mrefu zaidi.
Hilda alivunja rekodi ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na mpishi kutokea nchini India, Lata Tondon mwaka 2019 na rekodi hii ilivunjwa mapema hii leo saa moja na dakika 45 asubuhi alipotumia masaa 87 na dakika 45 mfululizo kupika vyakula zaidi ya 100 akilenga kutumia masaa 96 mfululizo ikiwa ni takriban siku nne.
Mwanamke huyo anatarajia kukamilisha lengo la masaa 96 ya kupika leo saa kumi na moja jioni kwa saa za Nigeria tangia aanze kupika Alhamisi ya wiki iliyopita.
Mpishi huyo ameonekana akiungwa mkono na watu wengi kutokea nchini Nigeria hasa watu mashuhuri na wanasiasa kutokea nchini humo wakiwemo mastaa kama Tiwa savage wakionekana katika hafla hiyo wikiendi hii.