Mke wa mshambuliaji wa Arsenal Kai Havertz amechapisha jumbe za matusi alizopokea kwenye mitandao ya kijamii wakati wa mechi ya Jumapili ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United, ikiwa ni pamoja na vitisho dhidi ya mtoto wake ambaye hajazaliwa.
Mshambuliaji huyo, 25, alikosa nafasi ya kushinda goli katika mchezo huo katika muda wa kawaida na kisha penalti yake ikaokolewa na kipa wa United, Altay Bayindir kwenye mikwaju ya penalti na United ikishinda 5-3 kwa penalti kufuatia sare ya 1-1.
Mke wa Mjerumani huyo Sophia alichapisha kwenye akaunti yake ya Instagram jumbe mbili alizopokea moja kwa moja kwenye mtandao huo.
Arsenal wameripoti matusi hayo kwa polisi na wanafanya kazi kwa kushirikiana na kampuni ya data ili kuwajua watuhumiwa.
“Mtu kufikiria kuwa ni sawa kuandika kitu kama hiki inanishtua sana. Aibu juu yako,” aliandika huku akiambatanisha picha ya ujumbe huo.
Wawili hao wamekuwa pamoja tangu 2018 na walifunga ndoa mwaka jana na Sophia alitangaza mwezi Novemba kuwa ni mjamzito.