Taarifa kutoka magharibi mwa Burundi katika Mkoa wa Cibitoke zinaeleza kuwa idadi kubwa ya wananchi eneo hilo wameshuhudiwa wakikimbia mkoa huo na kuelekea kwa wingi katika eneo la bonde la Ruzizi nchini DRC, kutokana na familia nyingi kukumbwa na baa la njaa.
Mamlaka katika eneo hilo imepanga kuelekea nje ya nchi kwa ajili ya kukutana na wananchi hao kuwashawishi kurejea nchini katika mazingira ambayo yanaonekana kuwa tishio ikiwa hali hiyo itaendelea kushuhudiwa.
Wananchi hao wengi wao ni kutoka katika tarafa za Gihanga, Mkoani Bubanza, Buganda na Rugombo Mkoani Cibitoke.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika eneo hilo zinaeleza kwamba hali hiyo ilianza kushuhudiwa tangu mwezi Julai mwaka huu.
Kadhalika sababu zingine ambazo zimeelezwa kufanya raia kuondoka, ni pamoja na uhasama mkubwa wa kaya unaochangiwa na kupungua kwa uwezo wa ununuzi.
Raia hao wamesemekana kupitia mto Rusizi unaounda mpaka wa nchi 2 kukimbilia Kongo, wengi wakihama nyakati za usiku wakivuka mto huo ambao umejaa mamba na viboko na hatari kubwa ya kuuawa na wanyama hawa.
Wale ambao walikuwa wamerejea nchini hivi karibuni kutoka Tanzania, Rwanda na DR Congo ni miongoni mwa watu hawa ambao bado wanarejea uhamishoni.