Miundombinu yote muhimu na wezeshi kwa ajili ya kuhudumia makasha (makontena) katika bandari kavu ya Kwala iliyopo iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani imeshakamilika na kuifanya bandari hiyo kavu kuwa na sifa zote na tayari kwa kuanza kazi.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Mei 27, 2023 na Meneja miliki wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Alexander Ndibalema akiongea na waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo na kusisitiza kuwa tayari bandari hiyo imeshasimikwa mifumo ya kimatandao ambayo inasomana moja kwa moja na bandari ya Dar es Salaam.
Ndibalema ameongeza kuwa, tayari katika bandari hiyo zipo ofisi za wadau wote bandari pamoja ofisi za kiforodha.
Ameendelea kwa kusema kuwa, bandari ya Kwala itakuwa ni mahususi kwa ajili ya kuhudumia makasha (makontena) yanayokwenda nchi jirani.
“Bandari kavu ya Kwala imeunganisha nchi jirani lengo likiwa ni kuhudumiwa makasha (makontena) yanayokwenda nchi jirani, tayari tumeshatenga maeneo maalum kwa kwa ajili ya nchi za Burundi, Rwanda, DR Congo ambapo kila nchi zimetengewa hekta kumi (10)
Ndibalema ametaja malengo ya kujenga bandari hiyo kuwa ni pamoja kupunguza msongamano wa mizigo na malori katika Bandari ya Dar es Salaam
“Lengo la Kujenga bandari kavu ya Kwala ni
.Kupunguza msongamano wa malori yanayoingia kutoka katika bandari ya Dar es Salaam
. Kuipunguzia mzigo bandari ya Dar es Salaam
. Kuwa chachu ya uwekezaji katika kongani ya Msafiri Pwani” alisisitiza Ndibalema
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kwala, Zaka Msafiri amesema, ujio wa bandari kavu ya Kwala imewanufaisha wakazi wa Kwala na maeneo jirani katika nyanja mbalimbali.
Mwenyekiti Msafiri ameyataja baadhi ya manufaa hayo kuwa ni pamoja na wananchi kupata ajira, kukuza biashara ,kuvutia uwekezaji pamoja na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kufuatia barabara yenye urefu wa kilometa 15.5 kujengwa ikiwa pia ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa bandari hiyo.
Nao Robert Francis na Jumanne Kibambe ambao ni wananchi wa kijiji cha Kwala wakiongea kwa nyakati tofauti wameishukuru serikali ya awamu sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza kwa kasi miradi yote muhimu na ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa bandari kavu ya Kwala ambapo
Bandari kavu ya Kwala inatarajiwa kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kuu la Kibiashara nchini.
Manufaa mtambuka ya bandari ya Kwala yatapelekea Tanzania kufunguka kiuchumi.