Mamlaka ya Usimamizi wa bandari Tanzania (TPA) kupitia bandari ya Tanga imeamua kuwa mdhamini mkuu wa maonyesho ya biashara ya Kimataifa “Tanga Trade Fair 2023” ili kujitangaza zaidi kwa wadau mbalimbali wanaoshiriki maonesho hayo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa kitengo cha masoko Bandari ya Tanga Bi Rose Tandiko wakati akimkaribisha Mgeni rasmi wa maonyesho hayo yanayo fanyika katika viwanja vya Mwahako Jijini Tanga, Kaimu Katibu Mkuu Kutoka Wizara ya Viwanda na biashara Bw Conrad Milinga wakati alipotembelea banda la bandari ya Tanga.
Bi Rose ameongeza kwa kusema kuwa bandari kama lango kuu la biashara imekua ikishiriki mara kwa mara maonyesho hayo ili kutoa elimu na kuonyesha huduma mbalimbali zinazotolewa na bandari ya Tanga kwa Wananchi na wadau wanaohudhiria maonyesho hayo.
Aliendelea kwa kusema kuwa kupitia maonyesho ya mwaka huu TPA watawafahamisha Wadau mbalimbali kuhusu mradi wa maboresho makubwa yaliofanywa katika bandari ya Tanga kutoka kuhudumua meli nangani km 1 mpaka gatini mradi ambao unakamilika hivi karibuni.